Job 30

1 a“Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki,
watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau
kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo.
2Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu,
kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia?
3 bWakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa,
walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa.
4 cKatika vichaka walikusanya mimea ya chumvi,
nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio.
5Walifukuzwa mbali na watu wao,
wakipigiwa kelele kama wevi.
6 dWalilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka,
kwenye majabali na mahandaki.
7 eKwenye vichaka walilia kama punda,
na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka.
8 fWao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya,
waliofukuzwa watoke katika nchi.

9 g“Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo;
nimekuwa kitu cha dhihaka kwao.
10 hWananichukia sana na kujitenga nami,
wala hawasiti kunitemea mate usoni.
11 iSasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa,
wamekuwa huru kunitendea waonavyo.
12 jKuume kwangu kundi linashambulia;
wao huitegea miguu yangu tanzi,
na kunizingira.
13 kHuizuia njia yangu,
nao hufanikiwa katika kuniletea maafa,
nami sina yeyote wa kunisaidia.
14Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana;
katikati ya magofu huja na kunishambulia.
15 lVitisho vimenifunika;
heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo,
salama yangu imetoweka kama wingu.

16 m“Sasa maisha yangu yamefikia mwisho;
siku za mateso zimenikamata.
17Usiku mifupa yangu inachoma;
maumivu yanayonitafuna hayatulii kamwe.
18Kwa uwezo wake mkuu Mungu huwa kwangu kama nguo;
hushikamana nami kama ukosi wa vazi langu.
19 nYeye amenitupa kwenye matope,
nami nimekuwa kama mavumbi na majivu.

20 o“Ee Bwana, ninakulilia wewe lakini hunijibu;
ninasimama, nawe unanitazama tu.
21 pWewe unanigeukia bila huruma;
unanishambulia kwa nguvu za mkono wako.
22 qUnaninyakua na kunipeperusha kwa upepo;
umenirusha huku na huko kwenye dhoruba kali.
23 rNinajua utanileta mpaka kifoni,
mahali ambapo wenye uhai wote wamewekewa.

24“Hakika hakuna yeyote amshambuliaye mhitaji,
anapoomba msaada katika shida yake.
25 sJe, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?
Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?
26 tLakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia;
nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.
27 uKusukwasukwa ndani yangu kamwe hakutulii;
siku za mateso zinanikabili.
28 vNinazunguka nikiwa nimeungua, lakini si kwa jua;
ninasimama katika kusanyiko nikiomba msaada.
29 wNimekuwa ndugu wa mbweha,
rafiki wa mabundi.
30 xNgozi yangu imekuwa nyeusi nayo inachunika;
mifupa yangu inaungua kwa homa.
31 yKinubi changu kimegeuka kuwa maombolezo,
nayo filimbi yangu imekuwa sauti ya kilio.
Copyright information for SwhNEN