Judges 1

Israeli Wapigana Na Wakanaani Waliobaki

1 aBaada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli wakamuuliza Bwana, “Ni nani atakayetangulia kupanda mbele yetu kwa ajili ya kupigana na Wakanaani?”

2 b Bwana akajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia; nimewapa hiyo nchi mikononi mwao.”

3Ndipo watu wa Yuda wakawaambia Wasimeoni ndugu zao, “Pandeni pamoja nasi katika nchi tuliyopewa, ili tupate kupigana na Wakanaani. Sisi pia tutakwenda pamoja nanyi katika sehemu yenu mliyopewa.” Basi Wasimeoni wakaenda pamoja nao.

4 cYuda aliposhambulia, Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, nao wakawaua watu 10,000 huko Bezeki. 5Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafanya Wakanaani na Waperizi wakimbie. 6Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuata na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu.

7 dNdipo Adoni-Bezeki akasema, “Nimewatendea wafalme sabini kama nilivyotendewa na kuwalisha makombo ya chakula chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya, kama yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.

8 eWatu wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto.

9 fBaada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, yaani, Negebu na nchi chini ya vilima vya magharibi. 10 gYuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (ambayo hapo kwanza iliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.

11 hKutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (ambao hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi.) 12Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” 13Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda, kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa akaolewa naye.

14Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”

15 iAkamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.

16 j kWazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Mose, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende,
Yaani Yeriko.
wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa jangwa ya Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi.

17 mBasi watu wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao kushambulia Wakanaani waishio Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma
Horma maana yake ni Maangamizi.
18 oWatu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka.

19 p Bwana alikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya chuma. 20 qKama vile Mose alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki. 21 rHata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wanaishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.

22 sBasi nyumba ya Yosefu wakashambulia Betheli, naye Bwana alikuwa pamoja nao. 23 tWalipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo kwanza uliitwa Luzu), 24 uwale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuonyeshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.” 25 vHivyo akawaonyesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote. 26 wYule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambao ndio jina lake hadi leo.

27 xLakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na vijiji vyake, au watu wa Taanaki na vijiji vyake, au watu wa Dori na vijiji vyake, au watu wa Ibleamu na vijiji vyake, au watu wa Megido na vijiji vyake, lakini Wakanaani waliazimu kuishi katika nchi ile. 28 yIsraeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa. 29 zWala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi humo miongoni mwao. 30Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, wala walioishi Nahaloli, ambao walibaki miongoni mwao; bali waliwatia katika kazi ya kulazimishwa. 31 aaWala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu 32na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi. 33 abWala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa. 34 acWaamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, kwa maana hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare. 35 adWaamori pia wakaendelea kukaa katika Mlima Heresi, katika Aiyaloni na Shaalbimu, lakini mkono wa nyumba ya Yosefu ukawalemea, nao wakashindwa hata wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa. 36 aeMpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.

Copyright information for SwhNEN