Luke 4:1-13

Yesu Ajaribiwa Na Shetani

(Mathayo 4:1-11; Marko 1:12-13)

1 aYesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi nyikani, 2 bmahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.

3 cIbilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”

4 dYesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’ ”

5 eIbilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja. 6 fAkamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka. 7Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”

8 gYesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ”

9 hKisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa, 10 ikwa maana imeandikwa:

“ ‘Atakuagizia malaika zake
ili wakulinde;
11 jnao watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”
12 kYesu akamjibu, “Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

13 lIbilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao.

Copyright information for SwhNEN