Matthew 24

Kubomolewa Kwa Hekalu Kwatabiriwa

(Marko 13:1-2; Luka 21:5-6)

1 aYesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2 bNdipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”

Ishara Za Nyakati Za Mwisho

(Marko 13:3-23; Luka 21:7-24)

3 cYesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”

4 dYesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5 eKwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’
Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
nao watawadanganya wengi.
6 gMtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. 7 hTaifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

9 i “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10 jWakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 kWatatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, 13 llakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 14 mInjili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.

15 n “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), 16basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. 17 oYeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. 18Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. 19 pOle wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! 20 qOmbeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. 21 rKwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe. 22 sKama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa. 23 tWakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. 24 uKwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.

26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 vKwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 wKwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

Kuja Kwa Mwana Wa Adamu

(Marko 13:24-31; Luka 21:25-33)

29 x “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

“ ‘jua litatiwa giza,
nao mwezi hautatoa nuru yake;
nazo nyota zitaanguka kutoka angani,
na nguvu za anga zitatikisika.’
30 y “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. 31 zNaye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

32 aa “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 33 abVivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. 34 acAmin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 35 adMbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa

(Marko 13:32-37; Luka 17:26-30, 34-36)

36 ae “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 afKama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38 agKwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. 39 ahNao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. 40 aiWatu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 41 ajWanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.

42 ak “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. 43 alLakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. 44 amKwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.

Mfano Wa Mtumishi Mwaminifu

(Luka 12:41-48)

45 an “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46 aoHeri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47 apAmin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48 aqLakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 arkisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 asAtamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

Copyright information for SwhNEN