Matthew 4:1-11

Kujaribiwa Kwa Yesu

(Marko 1:12-13; Luka 4:1-13)

1 aKisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 bBaada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 cMjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

4 dLakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

5 eNdipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, 6 fakamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:

“ ‘Atakuagizia malaika zake,
nao watakuchukua mikononi mwao
ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”
7 gYesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

8Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

10 hYesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”

11 iNdipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.

Copyright information for SwhNEN