1 Peter 1

Salamu

1 aPetro, mtume wa Yesu Kristo:

Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia.
2 bNi ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utiifu kwa Yesu Kristo na kunyunyiziwa damu yake:

Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi.

Tumaini Lenye Uzima

3 cAhimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 dili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 eninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6 fKatika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7 gHaya yamewajia ili kwamba imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto, ionekane kuwa halisi na imalizie katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atadhihirishwa. 8 hIngawa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9 iMaana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

10 jKwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, 11 kwakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. 12 lWalidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.

Mwito Wa Kuishi Maisha Matakatifu

13 mKwa hiyo, tayarisheni nia zenu kwa kazi; mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14 nKama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya wakati mlipoishi kwa ujinga. 15 oBali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, nanyi kuweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. 16 pKwa maana imeandikwa: “Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

17 qKwa sababu mnamwita Baba ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18 rKwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu, 19 sbali kwa damu ya thamani ya Kristo, yule Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20 tYeye alichaguliwa kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. 21 uKupitia kwake mmemwamini Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu ziwe kwa Mungu.

22 vBasi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli hata mkawa na upendo wa ndugu usio na unafiki, basi pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23 wKwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kupitia kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu milele. 24 xMaana,

“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao ni kama maua ya kondeni;
majani hunyauka na maua huanguka,
25 ylakini neno la Bwana ladumu milele.”
Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.

Copyright information for SwhNEN