1 Samuel 27
Daudi Miongoni Mwa Wafilisti
1Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka popote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.”2 aHivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi. 3 bDaudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali. 4Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena.
5Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko. Kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?”
6 cHivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo. 7 dDaudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne.
8 eBasi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia iteremkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.) 9 fKila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ngʼombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi.
10 gAkishi alipomuuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda,” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli,” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.” 11Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana Daudi aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’ ” Hii ndiyo ilikuwa desturi yake wakati wote aliishi katika nchi ya Wafilisti. 12 hAkishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.”
Copyright information for
SwhNEN