Acts 21

Paulo Aenda Yerusalemu

1 aTulipokwisha kujitenga nao, tukaanza safari kwa njia ya bahari moja kwa moja mpaka Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukaenda Patara. 2 bHapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo. 3 cTulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri mpaka Shamu, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake. 4 dBaada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. 5 eLakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba. 6 fBaada ya kuagana, tukapanda melini, nao wakarudi majumbani mwao.

7 gTukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja. 8 hSiku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake. 9 iFilipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.

10 jBaada ya kukaa kwa siku kadhaa, akateremka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo. 11 kAlipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’ ”

12Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13 lLakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.” 14 mAlipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”

15 nBaada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu. 16 oBaadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani kwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.

Kukamatwa Kwa Paulo, Na Safari Yake Kwenda Rumi

(21:17–28:31)

Paulo Awasili Yerusalemu

17 pTulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18 qKesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwepo. 19 rBaada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.

20 sBaada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria. 21 tLakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Mose, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu. 22Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu. 23 uKwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24 vJiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria. 25 wLakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”

26 xNdipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Paulo Akamatwa

27 yZile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka sehemu za Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata. 28 zWakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.” 29 aa(Walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini pamoja na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)

30 abMji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa. 31Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko. 32 acMara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari wakakimbilia kwenye ile ghasia, wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.

33 adYule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini. 34 aeBaadhi ya watu katika ule umati wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi. 35 afPaulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za ule umati wa watu zilikuwa kubwa. 36 agUmati wa watu ulikuwa ukifuata ukiendelea kupiga kelele ukisema, “Mwondoe huyu!”

Paulo Anajitetea

37 ahMara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?”

Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani?
38 aiJe, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi 4,000 wenye silaha jangwani?”

39 ajPaulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, huko Kilikia, raiya wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”

40 akAkiisha kupata ruhusa ya yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza kimya, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:

Copyright information for SwhNEN