Ecclesiastes 1

Kila Kitu Ni Ubatili Mtupu

1 aManeno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu:

2 b“Ubatili mtupu! Ubatili mtupu!”
Mhubiri anasema.
“Ubatili mtupu!
Kila kitu ni ubatili.”

3 cMwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote
anayotaabikia chini ya jua?
4 dVizazi huja na vizazi hupita,
lakini dunia inadumu milele.
5 eJua huchomoza na jua huzama,
nalo huharakisha kurudi mawioni.
6Upepo huvuma kuelekea kusini
na kugeukia kaskazini,
hurudia mzunguko huo huo,
daima ukirudia njia yake.
7 fMito yote hutiririka baharini,
hata hivyo bahari kamwe haijai.
Mahali mito inapotoka,
huko hurudi tena.
8 gVitu vyote vinachosha,
zaidi kuliko mtu anavyoweza kusema.
Jicho kamwe halitosheki kutazama,
wala sikio halishibi kusikia.
9 hKile kilichokuwepo kitakuwepo tena,
kile kilichofanyika kitafanyika tena,
hakuna kilicho kipya chini ya jua.
10Kuna kitu chochote ambacho mtu anaweza kusema,
“Tazama! Kitu hiki ni kipya”?
Kilikuwepo tangu zamani za kale,
kilikuwepo kabla ya wakati wetu.
11 iHakuna kumbukumbu ya watu wa zamani,
hata na wale ambao hawajaja bado
hawatakumbukwa
na wale watakaofuata baadaye.

Hekima Ni Ubatili

12Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli katika Yerusalemu. 13 jNilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu! 14 kNimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo.

15 lKilichopindika hakiwezi kunyooshwa,
kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.
16 mNiliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko yeyote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.” 17 nNdipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo.

18 oKwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa;
maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.
Copyright information for SwhNEN