Exodus 12

Pasaka

1 Bwana akamwambia Mose na Aroni katika nchi ya Misri, 2 a“Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu. 3 bIambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba. 4Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu. 5 cWanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. 6 dTunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni. 7 eNdipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao. 8 fUsiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu. 9 gMsile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani. 10 hMsibakize nyama yoyote mpaka asubuhi; nazo kama zitabakia mpaka asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto. 11 iHivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya Bwana.

12 j“Usiku huo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumuua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Bwana. 13 kDamu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.

14 l“Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu, mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwa Bwana, katika vizazi vyenu vyote: mtaishika kuwa amri ya kudumu. 15 mKwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana yeyote atakayekula chochote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka Israeli. 16 nKatika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.

17 o“Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa amri ya kudumu. 18 pKatika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja. 19 qKwa muda wa siku saba isionekane chachu yoyote katika nyumba zenu. Yeyote alaye chochote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa. 20 rMsile chochote kilichotiwa chachu. Popote muishipo, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”

21 sNdipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka. 22 tChukueni kitawi cha hisopo, kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi. 23 uBwana apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.

24“Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. 25 vMtakapoingia katika nchi Bwana atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26 wWatoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’ 27 xBasi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ” Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu. 28Waisraeli wakafanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni.

29 yIlipofika usiku wa manane, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia. 30 zFarao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.

Kutoka

31 aaWakati huo Farao akawaita Mose na Aroni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni kwa watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu Bwana kama mlivyoomba. 32 abChukueni makundi yenu ya kondoo na mbuzi pamoja na ngʼombe, kama mlivyosema, nanyi mwende zenu. Nanyi pia mnibariki.”

33 acWamisri wakawahimiza Waisraeli waondoke kwa haraka na kuacha nchi yao. Kwa kuwa walisema, “La sivyo, tutakufa wote!” 34Hivyo watu wakachukua donge lao la unga kabla ya kutiwa chachu, wakaweka ndani ya mabakuli ya kukandia, wakayaviringisha katika vitambaa na kuyabeba mabegani mwao. 35 adWaisraeli wakafanya kama Mose alivyowaelekeza, nao wakawaomba Wamisri wawapatie vitu vya fedha, dhahabu na nguo. 36 aeBasi Bwana alikuwa amewafanya Wamisri kuwa wakarimu kwa hawa watu, wakawapatia Waisraeli vile walivyotaka kwao; kwa hiyo wakawateka nyara Wamisri.

37 afWaisraeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi. Walikuwepo wanaume wapatao 600,000 waendao kwa miguu bila kuhesabu wanawake na watoto. 38 agWatu wengine wengi wakafuatana nao, pamoja na makundi makubwa ya mifugo wakiwemo kondoo, mbuzi na ngʼombe. 39 ahWakatengeneza maandazi yasiyotiwa chachu kwa ule unga uliokandwa waliokuwa wameutoa Misri, donge hilo la unga halikuwa limetiwa chachu, kwa kuwa walikuwa wameondolewa Misri kwa haraka nao hawakuwa na muda wa kuandaa chakula chao.

40 aiWaisraeli walikuwa wameishi Misri kwa muda wa miaka 430. 41 ajIlikuwa ni siku ya mwisho ya hiyo miaka 430, vikosi vyote vya Bwana vilipokuwa vimeondoka Misri. 42 akKwa sababu Bwana aliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri, katika usiku huu Waisraeli wote wanapaswa kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimu Bwana katika vizazi vijavyo.

Masharti Kwa Ajili Ya Pasaka

43 al Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Haya ndiyo masharti kwa ajili ya Pasaka:

“Mgeni hataruhusiwa kula Pasaka.
44 amMtumwa yeyote ambaye mmemnunua aweza kuila kama mmemtahiri, 45 anlakini kibarua yeyote au msafiri haruhusiwi kula.

46 ao“Sharti iliwe ndani ya nyumba; msichukue nyama yoyote nje ya nyumba hiyo. Msiuvunje mfupa wowote. 47Jumuiya yote ya Israeli ni lazima waiadhimishe Pasaka hiyo.

48 ap“Mgeni aishiye miongoni mwenu ambaye anataka kuadhimisha Pasaka ya Bwana ni lazima wanaume wote waliomo nyumbani mwake wawe wametahiriwa, ndipo aweze kushiriki kama mzawa. Mwanaume yeyote asiyetahiriwa haruhusiwi kuila. 49 aqSheria iyo hiyo itamuhusu mzawa na mgeni anayeishi miongoni mwenu.”

50Waisraeli wote walifanya kama vile Bwana alivyomwagiza Mose na Aroni. 51 arSiku ile ile Bwana akawatoa Waisraeli katika nchi ya Misri kwa vikosi vyao.

Copyright information for SwhNEN