Hosea 4

Shtaka Dhidi Ya Israeli

1 aSikieni neno la Bwana, enyi Waisraeli,
kwa sababu Bwana analo shtaka
dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:
“Hakuna uaminifu, hakuna upendo,
hakuna kumjua Mungu katika nchi.
2 bKuna kulaani tu, uongo na uuaji,
wizi na uzinzi,
bila kuwa na mipaka,
nao umwagaji damu mmoja
baada ya mwingine.
3 cKwa sababu hii nchi huomboleza,
wote waishio ndani mwake wanadhoofika,
wanyama wa kondeni, ndege wa angani
na samaki wa baharini wanakufa.

4 d“Lakini mtu awaye yote na asilete shtaka,
mtu yeyote na asimlaumu mwenzake,
kwa maana watu wako ni kama wale
waletao mashtaka dhidi ya kuhani.
5 eUnajikwaa usiku na mchana,
nao manabii hujikwaa pamoja nawe.
Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:
6 fwatu wangu wanaangamizwa
kwa kukosa maarifa,

“Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,
mimi nami nitakukataa wewe
usiwe kuhani kwangu mimi;
kwa kuwa umeacha kuijali sheria ya Mungu wako
mimi nami sitawajali watoto wako.
7 gKadiri makuhani walivyoongezeka,
ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu,
walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.
8 hHujilisha dhambi za watu wangu
na kupendezwa na uovu wao.
9 iHata itakuwa: Kama walivyo watu,
ndivyo walivyo makuhani.
Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao
na kuwalipa kwa matendo yao.

10 j“Watakula lakini hawatashiba;
watajiingiza katika ukahaba
lakini hawataongezeka,
kwa sababu wamemwacha Bwana
na kujiingiza wenyewe
11 kkatika ukahaba,
divai ya zamani na divai mpya,
ambavyo huondoa ufahamu
12 lwa watu wangu.
Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti
nao hujibiwa na fimbo ya mti.
Roho ya ukahaba imewapotosha,
hawana uaminifu kwa Mungu wao.
13 mWanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima
na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,
chini ya mialoni, milibua na miela,
ambako kuna vivuli vizuri.
Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba
na wake za wana wenu uzinzi.

14 n“Sitawaadhibu binti zenu wakati
wanapogeukia ukahaba,
wala wake za wana wenu
wanapofanya uzinzi,
kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya
na kutambikia pamoja na makahaba
wa mahali pa kuabudia miungu:
watu wasiokuwa na ufahamu
wataangamia!

15 o“Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli,
Yuda naye asije akawa na hatia.

“Usiende Gilgali,
usipande kwenda Beth-Aveni
Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka.

Wala usiape,
‘Hakika kama Bwana aishivyo!’
16 qWaisraeli ni wakaidi,
kama mtamba wa ngʼombe ambaye ni mkaidi.
Ni jinsi gani basi Bwana anaweza kuwachunga
kama wana-kondoo
katika shamba la majani?
17 rEfraimu amejiunga na sanamu,
ondokana naye!
18 sHata wakati wamemaliza vileo vyao
wanaendelea na ukahaba wao,
watawala wao hupenda sana
njia za aibu.
19 tKisulisuli kitawafagilia mbali
na dhabihu zao zitawaletea aibu.
Copyright information for SwhNEN