Isaiah 31
Ole Wa Wale Wanaotegemea Misri
1 aOle wao wale washukao Misri kwa ajili ya msaada,wale wategemeao farasi,
wanaoweka tumaini katika wingi wa magari yao ya vita,
na katika nguvu nyingi za wapanda farasi,
lakini hawamwangalii yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,
wala hawatafuti msaada kwa Bwana.
2 bHata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa,
wala hayatangui maneno yake.
Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu,
dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda mabaya.
3 cLakini Wamisri ni wanadamu, wala si Mungu,
farasi wao ni nyama, wala si roho.
Wakati Bwana atakaponyoosha Mkono wake,
yeye anayesaidia atajikwaa,
naye anayesaidiwa ataanguka,
wote wawili wataangamia pamoja.
4 dHili ndilo Bwana analoniambia:
“Kama vile simba angurumavyo,
simba mkubwa juu ya mawindo yake:
hata ingawa kundi lote la wachunga mifugo
huitwa pamoja dhidi yake,
hatiwi hofu na kelele zao
wala kusumbuliwa na ghasia zao;
ndivyo Bwana Mwenye Nguvu Zote atakavyoshuka
kufanya vita juu ya Mlima Sayuni
na juu ya vilele vyake.
5 eKama ndege warukao,
Bwana Mwenye Nguvu Zote ataukinga Yerusalemu;
ataukinga na kuuokoa,
atapita juu yake na kuufanya salama.”
6 fMrudieni yeye ambaye nyumba ya Israeli imemwasi sana. 7 gKwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi.
8 h“Ashuru itaanguka kwa upanga ambao si wa mwanadamu;
upanga usio wa kibinadamu utawaangamiza.
Watakimbia mbele ya upanga
na vijana wao wa kiume watafanyizwa kazi kwa lazima.
9 iNgome zao zitaanguka kwa sababu ya hofu;
kwa kuona bendera ya vita,
majemadari wao watashikwa na hofu ya ghafula,”
asema Bwana,
ambaye moto wake uko Sayuni,
nayo tanuru yake iko Yerusalemu.
Copyright information for
SwhNEN