Isaiah 64

1 aLaiti ungelipasua mbingu na kushuka chini,
ili milima ingelitetemeka mbele zako!
2 bKama vile moto uteketezavyo vijiti
na kusababisha maji kuchemka,
shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako,
na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako!
3 cKwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia,
ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako.
4 dTangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia,
hakuna sikio lililotambua,
hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe,
anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.
5 eUliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha,
wale wazikumbukao njia zako.
Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako,
ulikasirika.
Tutawezaje basi kuokolewa?
6 fSisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi,
nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu;
sisi sote tunasinyaa kama jani,
na kama upepo maovu yetu hutupeperusha.
7 gHakuna yeyote anayeliitia jina lako
wala anayejitahidi kukushika,
kwa kuwa umetuficha uso wako
na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu.

8 hLakini, Ee Bwana, wewe ndiwe Baba yetu.
Sisi ni udongo, wewe ndiye mfinyanzi;
sisi sote tu kazi ya mkono wako.
9 iEe Bwana, usikasirike kupita kiasi,
usizikumbuke dhambi zetu milele.
Ee Bwana, utuangalie, twakuomba,
kwa kuwa sisi sote tu watu wako.
10 jMiji yako mitakatifu imekuwa jangwa;
hata Sayuni ni jangwa, Yerusalemu ni ukiwa.
11 kHekalu letu takatifu na tukufu, mahali ambapo baba zetu walikusifu wewe,
limechomwa kwa moto,
navyo vitu vyote tulivyovithamini vimeharibika.
12 lEe Bwana, baada ya haya yote, utajizuia?
Je, utanyamaza kimya na kutuadhibu kupita kiasi?
Copyright information for SwhNEN