Jeremiah 10

Mungu Na Sanamu

1Sikieni lile ambalo Bwana, anena nanyi ee nyumba ya Israeli. 2 aHili ndilo asemalo Bwana:

“Usijifunze njia za mataifa
wala usitishwe na ishara katika anga,
ingawa mataifa yanatishwa nazo.
3 bKwa maana desturi za mataifa hazina maana,
wanakata mti msituni,
na fundi anauchonga kwa patasi.
4 cWanaparemba kwa fedha na dhahabu,
wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike.
5 dSanamu zao ni kama sanamu
iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege
nazo haziwezi kuongea;
sharti zibebwe
sababu haziwezi kutembea.
Usiziogope; haziwezi kudhuru,
wala kutenda lolote jema.”

6 eHakuna aliye kama wewe, Ee Bwana;
wewe ni mkuu,
jina lako ni lenye nguvu katika uweza.
7 fNi nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,
Ee Mfalme wa mataifa?
Hii ni stahili yako.
Miongoni mwa watu wote wenye hekima
katika mataifa na katika falme zao zote,
hakuna aliye kama wewe.
8 gWote hawana akili, tena ni wapumbavu,
wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote.
9 hHuleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi
na dhahabu kutoka Ufazi.
Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza
huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani:
vyote vikiwa vimetengenezwa
na mafundi stadi.
10 iLakini Bwana ni Mungu wa kweli,
yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele.
Anapokasirika, dunia hutetemeka,
mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
11 j“Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ”

12 kLakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,
akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,
na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
13 lAtoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,
naye huuleta upepo kutoka ghala zake.

14Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa,
kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.
Vinyago vyake ni vya udanganyifu,
havina pumzi ndani yavyo.
15 mHavifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha tu,
hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia.
16 nYeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,
kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,
pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:
Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

Maangamizi Yajayo

17 oKusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii,
enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
18 pKwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:
“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu
wote waishio katika nchi hii;
nitawataabisha
ili waweze kutekwa.”

19 qOle wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!
Jeraha langu ni kubwa!
Lakini nilisema,
“Kweli hii ni adhabu yangu,
nami sharti niistahimili.”
20 rHema langu limeangamizwa;
kamba zake zote zimekatwa.
Wana wangu wametekwa na hawapo tena;
hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu
wala wa kusimamisha kibanda changu.
21 sWachungaji hawana akili
wala hawamuulizi Bwana,
hivyo hawastawi
na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.
22 tSikilizeni! Taarifa inakuja:
ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!
Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa,
makao ya mbweha.

Maombi Ya Yeremia

23 uNinajua, Ee Bwana, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe;
hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
24 vUnirudi, Ee Bwana, lakini kwa kipimo cha haki:
si katika hasira yako,
usije ukaniangamiza.
25 wUmwage ghadhabu yako juu ya mataifa
wasiokujua wewe,
juu ya mataifa wasioliitia jina lako.
Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;
wamemwangamiza kabisa
na kuiharibu nchi yake.
Copyright information for SwhNEN