Job 39
1 a“Je, wajua ni wakati gani mbuzi wa mlimani wanapozaa?Je, watambua ni wakati gani kulungu jike azaapo mtoto wake?
2 bJe, waweza kuhesabu miezi hadi wazaapo?
Je, unajua majira yao ya kuzaa?
3Wao hujiinamisha na kuzaa watoto wao;
utungu wa kuzaa unakoma.
4Watoto wao hustawi na kuongezeka nguvu nyikani;
huenda zao wala hawarudi tena.
5 c“Ni nani aliyemwachia punda-mwitu awe huru?
Ni nani aliyezifungua kamba zake?
6 dNimempa nchi isiyokaliwa na watu kuwa masikani yake,
nchi ya chumvi kuwa makao yake.
7 eHuzicheka ghasia za mji,
wala hasikii kelele za mwendesha gari.
8 fHuzunguka vilimani kwa ajili ya malisho
na kutafuta kila kitu kibichi.
9 g“Je, nyati atakubali kukutumikia?
Atakaa karibu na hori lako usiku?
10 hJe, waweza kumfungia kwenye matuta kwa kamba?
Je, atalima mabonde nyuma yako?
11 iJe, utamtumainia kwa ajili ya nguvu zake nyingi?
Utamwachia yeye kazi zako nzito?
12Utaweza kumwamini akuletee nafaka yako nyumbani
kutoka shambani na kuikusanya kwenye sakafu yako ya kupuria?
13 j“Mbuni hupigapiga mabawa yake kwa furaha,
lakini hayawezi kulinganishwa
na mabawa na manyoya ya korongo.
14Huyataga mayai yake juu ya ardhi,
na kuyaacha yapate joto mchangani,
15 kbila kujali kuwa mguu waweza kuyaponda,
kwamba baadhi ya wanyama wa porini wanaweza kuyakanyaga.
16 lYeye huyafanyia makinda yake ukatili kama vile si yake;
hajali kwamba taabu yake inaweza ikawa bure,
17 mkwa kuwa Mungu hakumjalia hekima,
wala hakumpa fungu la akili njema.
18 nLakini akunjuapo mabawa yake kukimbia,
humcheka farasi pamoja na yeye aliyempanda.
19 o“Je, wewe humpa farasi nguvu
au kuivika shingo yake manyoya marefu?
20 pJe, wewe humfanya farasi aruke kama nzige,
akistaajabisha kwa tishio la mlio wake wa majivuno?
21 qHuparapara bila woga, akizifurahia nguvu zake,
husonga mbele kukabiliana na silaha.
22 rHuicheka hofu, haogopi chochote,
wala haukimbii upanga.
23 sPodo hutoa sauti kando yake,
pamoja na mkuki unaongʼaa na fumo.
24 tBila woga na kwa ghadhabu huimeza nchi,
wala tarumbeta iliapo yeye hawezi kusimama.
25 uAsikiapo sauti ya baragumu yeye hulia, ‘Aha!’
Hunusa harufu ya vita toka mbali,
sauti ya mtoa amri na ukelele wa vita.
26“Je, mwewe huruka kwa hekima yako
na kuyakunjua mabawa yake kuelekea kusini?
27Je, tai hupaa juu kwa amri yako
na kujenga kiota chake mahali pa juu?
28Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku;
majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake.
29Kutoka huko hutafuta chakula chake;
macho yake hukiona kutoka mbali.
30 vMakinda yake hujilisha damu,
na pale palipo na machinjo, ndipo yeye alipo.”
Copyright information for
SwhNEN