Job 4

Elifazi Anazungumza: Ayubu Ametenda Dhambi

1 aNdipo Elifazi Mtemani akajibu:

2 b“Kama mtu akithubutu kuzungumza nawe,
kutakukasirisha?
Lakini ni nani awezaye
kujizuia asiseme?
3 cFikiri jinsi ambavyo umewafundisha watu wengi,
jinsi ambavyo umeitia nguvu
mikono iliyokuwa dhaifu.
4 dManeno yako yamewategemeza wale waliojikwaa;
umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu.
5 eLakini sasa hii taabu imekujia wewe,
nawe unashuka moyo;
imekupiga wewe,
nawe unafadhaika.
6 fJe, kumcha Mungu kwako hakupaswi kuwa
ndiyo matumaini yako
na njia zako kutokuwa na lawama
ndilo taraja lako?

7 g“Fikiri sasa: Ni mtu yupi asiye na hatia ambaye aliwahi kuangamia?
Ni wapi wanyofu waliwahi kuangamizwa?
8 hKwa jinsi ambavyo mimi nimechunguza,
wale walimao ubaya
na wale hupanda uovu,
huvuna hayo hayo hayo.
9 iKwa pumzi ya Mungu huangamizwa;
kwa mshindo wa hasira zake huangamia.
10 jSimba anaweza kunguruma na kukoroma,
lakini bado meno ya simba mkubwa huvunjika.
11 kSimba anaweza kuangamia kwa kukosa mawindo,
nao wana wa simba jike hutawanyika.

12 l“Neno lililetwa kwangu kwa siri,
masikio yangu yakasikia mnongʼono wake.
13 mKatikati ya ndoto za kutia wasiwasi wakati wa usiku,
hapo usingizi mzito uwapatapo wanadamu,
14 nhofu na kutetemeka kulinishika
na kufanya mifupa yangu yote itetemeke.
15 oKuna roho aliyepita mbele ya uso wangu,
nazo nywele za mwili wangu zikasimama.
16 pYule roho akasimama,
lakini sikuweza kutambua kilikuwa kitu gani.
Umbo fulani lilisimama mbele ya macho yangu,
kukawa na ukimya kisha nikasikia sauti:
17 q‘Je, binadamu aweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu?
Je, mtu aweza kuwa safi kuliko Muumba wake?
18 rKama Mungu hawaamini watumishi wake,
kama yeye huwalaumu malaika zake kwa kukosea,
19 sni mara ngapi zaidi wale waishio katika nyumba
za udongo wa mfinyanzi,
ambazo misingi yake ipo mavumbini,
ambao wamepondwa kama nondo!
20 tKati ya mawio na machweo
huvunjwa vipande vipande;
bila yeyote kutambua,
huangamia milele.
21 uJe, kamba za hema yao hazikungʼolewa,
hivyo hufa bila hekima?’
Copyright information for SwhNEN