Judges 4

Debora

1 aBaada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakafanya tena maovu machoni pa Bwana. 2 bHivyo Bwana akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori. Jemadari wa jeshi lake alikuwa Sisera, aliyeishi huko Haroshethi-Hagoyimu
Haroshethi-Hagoyimu ina maana Haroshethi ya Mataifa.
3 dKwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma yapatayo 900, naye alikuwa amewatesa Waisraeli kwa ukatili kwa muda wa miaka ishirini, Waisraeli wakamlilia Bwana wakaomba msaada.

4 eDebora, nabii mwanamke, mkewe Lapidothi, ndiye alikuwa anaamua Israeli wakati ule. 5 fDebora alikuwa akiketi chini ya Mtende wa Debora uliokuwa kati ya Rama na Betheli katika nchi ya vilima ya Efraimu, nao Waisraeli wakaja kwake ili awaamue. 6 gAkatuma wamwite Baraka mwana wa Abinoamu kutoka Kedeshi huko Naftali na kumwambia, “Bwana, Mungu wa Israeli, anakuagiza: ‘Nenda, chukua wanaume 10,000 toka Naftali na Zabuloni, mwende Mlima Tabori. 7 hNitamshawishi Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, pamoja na magari yake na jeshi lake, hadi Mto Kishoni na kumtia mikononi mwako.’ ”

8Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami nitakwenda, lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.”

9 iDebora akamwambia, “Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini njia unayoiendea haitakupa heshima wewe, kwa kuwa Bwana atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Hivyo Debora akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi, 10 jmahali ambapo Baraka aliwaita Zabuloni na Naftali. Watu 10,000 wakamfuata Baraka, na Debora pia akaenda pamoja naye.

11 kBasi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wengine, yaani, wazao wa Hobabu, mkwewe Mose, naye akapiga hema lake karibu na ule mti mkubwa wa mwaloni ulioko Saananimu, karibu na Kedeshi.

12 lSisera alipoambiwa kuwa Baraka mwana wa Abinoamu alikuwa amepanda Mlima Tabori, 13 mSisera akakusanya pamoja magari yake yote 600 ya chuma na watu wote waliokuwa pamoja naye, kuanzia Haroshethi-Hagoyimu mpaka Mto wa Kishoni.

14 nNdipo Debora akamwambia Baraka, “Nenda! Hii ndiyo siku ambayo Bwana amemtia Sisera mikononi mwako. Je, Bwana hakukutangulia mbele yako?” Hivyo Baraka akashuka kutoka Mlima Tabori, akifuatwa na watu 10,000. 15 oBwana akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, pamoja na jeshi lake lote kwa upanga mbele ya Baraka, naye Sisera akaliacha gari lake na kukimbia kwa miguu. 16 pLakini Baraka akafuata magari pamoja na jeshi mpaka Haroshethi-Hagoyimu. Jeshi lote la Sisera likaanguka kwa upanga, wala hakuna hata mtu mmoja aliyesalia.

17 qSisera, hata hivyo, akakimbia kwa miguu mpaka kwenye hema la Yaeli, mkewe Heberi, Mkeni, kwa sababu palikuwa na uhusiano wa kirafiki kati ya Yabini mfalme wa Hazori na ukoo wa Heberi, Mkeni.

18Yaeli akaenda kumlaki Sisera na kumwambia, “Karibu, bwana wangu, karibu ingia ndani kabisa. Usiogope.” Basi Sisera akaingia ndani ya hema ya Yaeli, naye akamfunika kwa blanketi nene.

19 rAkamwambia, “Nina kiu, tafadhali nipe maji ya kunywa.” Ndipo akafungua kiriba cha maziwa na kumpa akanywa, kisha akamfunika.

20Naye Sisera akamwambia, “Simama mlangoni pa hema na mtu yeyote akija na kukuuliza, ‘Je, kuna mtu yeyote hapa?’ sema, ‘Hapana.’ ”

21 sNdipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akachukua nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akiwa amelala usingizi, akiwa amechoka. Akakigongomea kile kigingi kwenye paji la uso wake, kikapenya hata kuingia ardhini, naye akafa.

22 tBaraka akakaribia akimfuatia Sisera, Yaeli akatoka kumlaki. Akamwambia, “Njoo, nitakuonyesha mtu unayemtafuta.” Hivyo wakaingia ndani ya hema wakiwa wamefuatana na tazama Sisera alikuwa amelala humo, akiwa amekufa, na hicho kigingi cha hema kikiwa kimegongomewa kupitia paji la uso wake.

23 uBasi siku ile Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani, mbele ya Israeli. 24 vNao mkono wa Waisraeli ukaendelea kuwa na nguvu zaidi na zaidi dhidi ya Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka wakamwangamiza.

Copyright information for SwhNEN