Luke 9:10-17
Yesu Awalisha Wanaume 5,000
(Mathayo 14:13-21; Marko 6:30-44; Yohana 6:1-14)
10 aMitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji uitwao Bethsaida. 11 bLakini umati wa watu ukafahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.12 cIlipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Yesu na kumwambia, “Waage makutano ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”
13Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”
Nao wakajibu, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.” 14Walikuwako wanaume wapatao 5,000.
Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.” 15Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. 16 dYesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu. 17Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.
Copyright information for
SwhNEN