Matthew 14:1-12
Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa
(Marko 6:14-29; Luka 9:7-9)
1 aWakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Yesu, 2 bakawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”3 cHerode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, 4 dkwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” 5 eHerode alitaka sana kumuua Yohana, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.
6Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti wa Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria, akamfurahisha sana Herode, 7kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. 8Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” 9Mfalme akasikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. 10 fHivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. 11Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. 12 gWanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.
Copyright information for
SwhNEN