Micah 3
Viongozi Na Manabii Wakemewa
1 aKisha nikasema,“Sikilizeni enyi viongozi wa Yakobo,
enyi watawala wa nyumba ya Israeli.
Je, hampaswi kujua hukumu,
2 bninyi mnaochukia mema
na kupenda maovu;
ninyi mnaowachuna watu wangu ngozi
na kuondoa nyama kwenye mifupa yao;
3 cninyi mnaokula nyama ya watu wangu,
mnaowachuna ngozi
na kuvunja mifupa yao vipande vipande;
mnaowakatakata kama nyama
ya kuwekwa kwenye sufuria
na kama nyama
ya kuwekwa kwenye chungu?”
4 dKisha watamlilia Bwana,
lakini hatawajibu.
Wakati huo atawaficha uso wake
kwa sababu ya uovu waliotenda.
5 eHili ndilo asemalo Bwana:
“Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu,
mtu akiwalisha,
wanatangaza ‘amani’;
kama hakufanya hivyo,
wanaandaa kupigana vita dhidi yake.
6 fKwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono,
na giza, msiweze kubashiri.
Jua litawachwea manabii hao,
nao mchana utakuwa giza kwao.
7 gWaonaji wataaibika
na waaguzi watafedheheka.
Wote watafunika nyuso zao
kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”
8 hLakini kuhusu mimi, nimejazwa nguvu,
nimejazwa Roho wa Bwana,
haki na uweza,
kumtangazia Yakobo kosa lake,
na Israeli dhambi yake.
9 iSikieni hili, enyi viongozi wa nyumba ya Yakobo,
enyi watawala wa nyumba ya Israeli,
mnaodharau haki
na kupotosha kila lililo sawa;
10 jmnaojenga Sayuni kwa kumwaga damu
na Yerusalemu kwa uovu.
11 kViongozi wake wanahukumu kwa rushwa,
na makuhani wake wanafundisha kwa malipo,
nao manabii wake wanatabiri kwa fedha.
Hata hivyo wanamwegemea Bwana na kusema,
“Je, Bwana si yumo miongoni mwetu?
Hakuna maafa yatakayotupata.”
12 lKwa hiyo kwa sababu yenu,
Sayuni italimwa kama shamba,
Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto,
na kilima cha Hekalu
kitakuwa kichuguu
kilichofunikwa na vichaka.
Copyright information for
SwhNEN