Numbers 30

Nadhiri

1 aMose akawaambia viongozi wa makabila ya Israeli: “Hili ndilo Bwana analoagiza: 2 bMwanaume awekapo nadhiri kwa Bwana, au anapoapa kujifunga kwa ahadi, kamwe asitangue neno lake, bali ni lazima afanye kila kitu alichosema.

3“Wakati mwanamwali anayeishi bado nyumbani kwa baba yake atakapoweka nadhiri kwa Bwana, ama amejifunga mwenyewe kwa ahadi, 4na baba yake akasikia kuhusu nadhiri au ahadi yake lakini asimwambie lolote, ndipo nadhiri zake zote na kila ahadi aliyoiweka na kujifunga kwayo itathibitika. 5Lakini kama baba yake akimkataza wakati anapoisikia, hakuna nadhiri wala ahadi yake yoyote aliyojifunga kwayo itakayosimama; Bwana atamweka huru huyo mwanamwali kwa sababu baba yake amemkataza.

6 c“Ikiwa ataolewa baada ya kuweka nadhiri au baada ya midomo yake kutamka ahadi fulani bila kufikiri akawa amejifunga hivyo, 7na mume wake akasikia habari hiyo asimwambie neno lolote, ndipo nadhiri zake ama ahadi zake ambazo alikuwa amejifunga nazo zitathibitika. 8 dLakini ikiwa mume wake atamkataza atakaposikia kuhusu hilo, atakuwa ametangua nadhiri ambazo zilikuwa zimemfunga mkewe, ama ahadi aliyotamka pasipo kufikiri ambayo amejifunga kwayo, naye Bwana atamweka huru yule mwanamke.

9 e“Nadhiri yoyote ama patano ambalo limefanywa na mjane ama mwanamke aliyeachwa vitakuwa vimemfunga.

10“Ikiwa mwanamke anayeishi na mumewe ataweka nadhiri ama kujifunga mwenyewe kwa ahadi chini ya kiapo, 11na mumewe akasikia kuhusu jambo hili lakini asimwambie lolote wala hakumkataza, ndipo viapo vyake vyote au ahadi zinazomfunga zitakapothibitika. 12 fLakini ikiwa mumewe atabatilisha nadhiri hizo baada ya kuzisikia, basi hakuna nadhiri au ahadi zozote alizoziweka kwa midomo yake zitakazothibitika. Mumewe atakuwa amezibatilisha, na Bwana atamweka huru yule mwanamke. 13Mumewe anaweza kuthibitisha au kutangua nadhiri yoyote anayoweka, au ahadi yoyote aliyoweka kwa kuapa ili kujikana mwenyewe. 14Lakini ikiwa mumewe hasemi lolote kwake kuhusu jambo hilo siku baada ya siku, basi mumewe atakuwa amethibitisha nadhiri zote, na ahadi zote zinazomfunga mkewe. Anavithibitisha kwa kutokusema lolote kwa mkewe anapoyasikia hayo. 15Hata hivyo, ikiwa mumewe atavibatilisha baada ya kusikia hayo, basi atawajibika kwa hatia ya mkewe.”

16Haya ndiyo masharti ambayo Bwana alimpa Mose kuhusu mahusiano kati ya mtu na mkewe, na kati ya baba na binti yake ambaye bado anaishi nyumbani kwa baba yake.

Copyright information for SwhNEN