Song of Solomon 2

Mpendwa

1 aMimi ni ua la Sharoni,
yungiyungi ya bondeni.
Mpenzi

2Kama yungiyungi katikati ya miiba
ndivyo alivyo mpenzi wangu katikati ya wanawali.
Mpendwa

3 bKama mti wa mtofaa miongoni mwa miti ya msituni
ndivyo alivyo mpenzi wangu
miongoni mwa wanaume vijana.
Ninafurahia kuketi kivulini mwa mwanaume huyu,
na tunda lake ni tamu kwangu.
4 cAmenichukua mpaka kwenye ukumbi wa karamu,
na bendera ya huyu mwanaume
juu yangu ni upendo.
5 dNitie nguvu kwa zabibu kavu,
niburudishe kwa matofaa,
kwa maana ninazimia kwa mapenzi.
6 eMkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,
na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
7 fBinti za Yerusalemu, ninawaagiza
kwa paa na kwa ayala wa shambani:
Msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.

Shairi La Pili

Mpendwa

8 gSikiliza! Mpenzi wangu!
Tazama! Huyu hapa anakuja,
akirukaruka juu milimani
akizunguka juu ya vilima.
9 hMpenzi wangu ni kama paa au ayala kijana.
Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu,
akitazama kupitia madirishani,
akichungulia kimiani.
10Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia,
“Inuka, mpenzi wangu,
mrembo wangu, tufuatane.
11Tazama! Wakati wa masika umepita,
mvua imekwisha na ikapita.
12Maua yanatokea juu ya nchi;
majira ya kuimba yamewadia,
sauti za njiwa zinasikika
katika nchi yetu.
13 i jMtini unatunga matunda yake ya mwanzoni,
zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri.
Inuka, njoo mpenzi wangu.
Mrembo wangu, tufuatane.”
Mpenzi

14 kHua wangu penye nyufa za majabali,
mafichoni pembezoni mwa mlima,
nionyeshe uso wako,
na niisikie sauti yako,
kwa maana sauti yako ni tamu,
na uso wako unapendeza.
15 lTukamatie mbweha,
mbweha wale wadogo
wanaoharibu mashamba ya mizabibu,
mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua.
Mpendwa

16 mMpenzi wangu ni wangu, nami ni wake,
yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.
17 nMpaka jua linapochomoza,
na vivuli vikimbie,
rudi, mpenzi wangu,
na uwe kama paa,
au kama ayala kijana
juu ya vilima vya Betheri.
Copyright information for SwhNEN