Esther 4

Mordekai Amshawishi Esta Kusaidia

1 aMordekai alipojua yote yaliyokwisha kufanyika, alirarua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia na kujipaka majivu, akaenda mjini, akiomboleza kwa sauti na kwa uchungu. 2Alikwenda akasimama nje ya lango la mfalme, kwa sababu hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia akiwa amevaa nguo za magunia. 3Katika kila jimbo ambapo amri na agizo la mfalme lilifika, kulikuwa na maombolezo makuu miongoni mwa Wayahudi pamoja na kufunga, kulia na kuomboleza. Watu wengi wakalala juu ya nguo za magunia na majivu.

4Wajakazi wa Esta na matowashi walipokuja na kumwambia kuhusu Mordekai, alipatwa na huzuni kuu. Alimtumia nguo avae badala ya nguo za magunia, lakini Mordekai hakuzikubali. 5Ndipo Esta akamwita Hathaki, mmojawapo wa matowashi wa mfalme ambaye alikuwa amewekwa kumhudumia Esta, akamwagiza kutafuta ni nini kilikuwa kikimtaabisha Mordekai na ni kwa nini.

6Basi Hathaki alitoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanja ulio wazi wa mji mbele ya lango la mfalme. 7 bMordekai akamwambia kila kitu ambacho kimempata, pamoja na hesabu kamili ya fedha ambazo Hamani aliahidi kulipa katika hazina ya mfalme kwa ajili ya maangamizi ya Wayahudi. 8Akampa nakala ya andiko la amri kwa ajili ya maangamizi yao, lililokuwa limechapishwa huko Shushani, kumwonyesha Esta na kumwelezea. Mordekai akamwambia towashi amshawishi Esta kwenda mbele ya mfalme kuomba rehema na kumsihi kwa ajili ya watu wake.

9Hathaki akarudi kwa Esta na kumwarifu alilolisema Mordekai. 10Kisha Esta akamwamuru Hathaki amweleze Mordekai, 11 c“Maafisa wote wa mfalme na watu wa majimbo ya ufalme wanajua kuwa mwanaume au mwanamke yeyote ambaye ataingia kumwona mfalme katika ua wa ndani bila kuitwa, mfalme ana sheria moja tu: Atauawa. Njia pekee kinyume na hili ni mfalme kumnyooshea fimbo ya dhahabu ili aishi. Lakini siku thelathini zimepita tangu nilipoitwa kwenda kwa mfalme.”

12Wakati Mordekai aliarifiwa maneno ya Esta, 13Mordekai alirudisha jibu hili: “Usifikiri kwamba kwa sababu uko katika nyumba ya mfalme wewe pekee katika Wayahudi wote utapona. 14 dKwa kuwa kama utakaa kimya wakati huu, msaada na ukombozi kwa Wayahudi utatoka mahali pengine, lakini wewe na jamaa ya baba yako mtaangamia. Nani ajuaye kwamba hukuja kwenye nafasi ya mamlaka kwa ajili ya wakati kama huu?”

15Kisha Esta alituma jibu hili kwa Mordekai: 16 e“Nenda, kusanya pamoja Wayahudi wote walioko Shushani, nanyi mfunge kwa ajili yangu. Msile wala kunywa kwa siku tatu, usiku na mchana. Mimi na wajakazi wangu tutafunga kama mnavyofanya. Baada ya kufanyika hili, nitakwenda kwa mfalme, hata ingawa ni kinyume cha sheria. Ikiwa ni kuangamia na niangamie.”

17Kwa hiyo Mordekai alikwenda zake na kutekeleza maagizo yote ya Esta.

Copyright information for SwhNEN