Exodus 13

Kuwekwa Wakfu Kwa Wazaliwa Wa Kwanza

BWANA akamwambia Mose, “Niwekeeni wakfu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kila mtoto wa kwanza aliye kifungua tumbo miongoni mwa Waisraeli ni mali yangu, akiwa wa mwanadamu au wa mnyama.”

Ndipo Mose akawaambia watu, “Ikumbukeni siku hii, siku ambayo mlitoka katika nchi ya Misri, katika nchi ya utumwa, kwa sababu BWANA aliwatoa humo kwa mkono wenye nguvu. Msile cho chote kilichotiwa chachu. Leo, katika mwezi wa Abibu
13.4 Abibu ni jina la mwezi wa kwanza kwa Wayahudi, ambao ni mwezi wa nne katika kalenda yetu
, mnatoka.
BWANA atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Wahivi na Wayebusi, nchi aliyowaapia baba zako kukupa, nchi itiririkayo maziwa na asali, utaiadhimisha sikukuu hii katika mwezi huu: Kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu na katika siku ya saba utamfanyia BWANA sikukuu. Kwa muda wa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu, pasionekane kitu cho chote kilicho na chachu miongoni mwako, wala chachu yo yote isionekane po pote ndani ya mipaka yako. Siku ile utamwambia mwanao, ‘Nafanya hivi kwa sababu ya jambo ambalo BWANA alinitendea nilipotoka katika nchi ya Misri.’ Adhimisho hili, litakuwa kama alama kwenye mkono wako na ukumbusho katika paji lako la uso, kwamba sheria ya BWANA inapaswa iwe kinywani mwako. Kwa kuwa BWANA alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu. 10 Ni lazima uishike amri hii kwa wakati uliopangwa mwaka baada ya mwaka.

11 “Baada ya BWANA kukuingiza katika nchi ya Wakanaani na kukupa nchi hiyo, kama alivyokuahidi kwa kiapo na kwa baba zako, 12 inakupasa kumtolea BWANA mzaliwa wa kwanza wa kila tumbo. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume wa mifugo yako ni mali ya BWANA. 13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo, lakini kama hukumkomboa, utamvunja shingo yake. Kila mzaliwa wa kwanza mwanaume miongoni mwa wana wenu utamkomboa.

14 “Katika siku zijazo, mwanao akikuuliza, ‘Hii ina maana gani?’ Mwambie, ‘Kwa mkono wenye nguvu BWANA alitutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa. 15 Farao alipokataa kwa ukaidi kuturuhusu kuondoka, BWANA aliua kila mzaliwa wa kwanza wa Wamisri, mwanadamu na wa mnyama. Hii ndiyo sababu ninatoa dhabihu kwa BWANA mzaliwa wa kwanza wa kiume, wa kila tumbo na kumkomboa kila mzaliwa wa kwanza wa wana wangu.’ 16 Jambo hili litakuwa kama ishara kwenye mkono wako na kama alama kwenye paji la uso wako, kwamba BWANA alikutoa katika nchi ya Misri kwa mkono wake wenye nguvu.”

Nguzo Ya Wingu Na Moto

17 Farao alipowaachia watu waende, Mungu hakuwaongoza kufuata njia ipitiayo katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa fupi zaidi. Kwa maana Mungu alisema, “Wakikabiliana na vita, wanaweza kubadili mawazo yao na kurudi Misri.” 18 Kwa hiyo Mungu akawaongoza watu kupitia njia ya kuzunguka kupitia jangwani, kuelekea Bahari ya Shamu. Waisraeli walipanda kutoka katika nchi ya Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.

19 Mose akachukua mifupa ya Yosefu kwa sababu Yosefu alikuwa amewaapisha wana wa Israeli. Alikuwa amewaambia, “Hakika Mungu atakuja kuwasaidia, nanyi ni lazima mwiichukue mifupa yangu mwende nayo kutoka mahali hapa.”

20 Baada ya Waisraeli kuondoka Sukothi wakapiga kambi huko Ethamu pembeni mwa jangwa. 21 Wakati wa mchana BWANA aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku. 22 Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.

Copyright information for Neno