Ezekiel 14

Waabudu Sanamu Walaumiwa

1 aBaadhi ya wazee wa Israeli walinijia na kuketi mbele yangu. 2Ndipo neno la Bwana likanijia kusema: 3 b“Mwanadamu, watu hawa wameweka sanamu katika mioyo yao na kuweka vitu viovu vya kukwaza mbele ya macho yao. Je, kweli niwaruhusu waniulize jambo lolote? 4Kwa hiyo sema nao uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Wakati Mwisraeli yeyote anapoweka sanamu moyoni mwake na kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akaenda kwa nabii, Mimi Bwana nitamjibu peke yangu sawasawa na ukubwa wa ibada yake ya sanamu. 5 cNitafanya jambo hili ili kukamata tena mioyo ya watu wa Israeli, ambao wote wameniacha kwa ajili ya sanamu zao.’

6 d“Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Tubuni! Geukeni kutoka kwenye sanamu zenu na mkatae matendo yenu yote ya machukizo!

7 e“ ‘Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote anayeishi katika Israeli anapojitenga nami na kujiwekea sanamu katika moyo wake na kwa hivyo kuweka kitu kiovu cha kukwaza mbele ya macho yake na kisha akamwendea nabii kuuliza shauri kwangu, mimi Bwana nitamjibu mwenyewe. 8 fNitaukaza uso wangu dhidi ya mtu huyo na kumwadhibu na kumfanya ishara kwa watu. Nitamkatilia mbali kutoka watu wangu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.

9 g“ ‘Naye nabii kama atakuwa ameshawishika kutoa unabii, Mimi Bwana nitakuwa nimemshawishi nabii huyo, nami nitaunyoosha mkono wangu dhidi yake na kumwangamiza kutoka miongoni mwa watu wangu Israeli. 10Watachukua hatia yao, nabii atakuwa na hatia sawa na yule mtu aliyekuja kuuliza neno kwake.

11 h“ ‘Ndipo watu wa Israeli hawataniacha tena, wala kujitia unajisi tena kwa dhambi zao zote. Ndipo watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao, asema Bwana Mwenyezi.’ ”

Hukumu Isiyoepukika

12Neno la Bwana likanijia kusema, 13 i“Mwanadamu, kama nchi itanitenda dhambi kwa kutokuwa waaminifu nami nikinyoosha mkono wangu dhidi yake kukatilia mbali upatikanaji wake wa chakula na kuipelekea njaa na kuua watu wake na wanyama wao, 14 jhata kama watu hawa watatu: Noa, Danieli na Ayubu wangekuwa ndani ya nchi hiyo, ndio hao tu wangeweza kujiokoa wenyewe kwa uadilifu wao, asema Bwana Mwenyezi.

15 k“Au kama nikipeleka wanyama pori katika nchi hiyo yote na kuifanya isiwe na watoto, nayo ikawa ukiwa kwamba hakuna mtu apitaye katika nchi hiyo kwa sababu ya wanyama pori, 16 lhakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao peke yao wangeokolewa, lakini nchi ingekuwa ukiwa.

17 m“Au kama nikileta upanga dhidi ya nchi hiyo na kusema, ‘Upanga na upite katika nchi yote,’ nami nikiua watu wake na wanyama wao, 18 nhakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hata kama watu hawa watatu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kuokoa wana wao wala binti zao. Wao wenyewe tu wangeokolewa.

19 o“Au kama nikipeleka tauni katika nchi hiyo na kumwaga ghadhabu yangu juu yake kwa njia ya kumwaga damu, kuua watu wake na wanyama wao, 20 phakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, hata kama Noa, Danieli na Ayubu wangekuwa humo ndani yake, wasingeweza kumwokoa mwana wala binti. Wao wangeweza kujiokoa wenyewe tu kwa uadilifu wao.

21 q“Kwa maana hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Itakuwa vibaya kiasi gani nitakapopeleka dhidi ya Yerusalemu hukumu zangu nne za kutisha, yaani, upanga, njaa, wanyama pori na tauni, ili kuua watu wake na wanyama wao! 22 rLakini watakuwepo wenye kuokoka, wana na binti wataletwa kutoka nje ya nchi hiyo. Watawajia ninyi, nanyi mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, mtafarijika kuhusu maafa niliyoleta juu ya Yerusalemu, kwa ajili ya yale yote niliyoleta juu yake. 23 sMtafarijika wakati mtakapoona mwenendo wao na matendo yao, kwa kuwa mtajua kwamba sikufanya lolote ndani yake bila sababu, asema Bwana Mwenyezi.”

Copyright information for SwhNEN