Job 5

Elifazi Anaendelea

1 a“Ita kama unataka, lakini ni nani atakayekujibu?
Ni yupi kati ya hao watakatifu utakayemgeukia?
2 bKuweka uchungu moyoni humuua mpumbavu,
nao wivu humchinja mjinga.
3 cMimi mwenyewe nimemwona mpumbavu akistawi,
lakini ghafula nyumba yake ikawa imelaaniwa.
4 dWatoto wake wako mbali na usalama,
hushindwa mahakamani bila mtetezi.
5 eWenye njaa huyala mavuno yake,
wakiyatoa hata katikati ya miiba,
nao wenye kiu huitamani sana mali yake.
6 fKwa maana taabu haioti kutoka kwenye udongo,
wala udhia hauchipui kutoka ardhini.
7 gLakini mwanadamu huzaliwa ili kutaabika,
kwa hakika kama cheche za moto zirukavyo kuelekea juu.

8 h“Lakini ingekuwa ni mimi, ningemlalamikia Mungu,
ningeliweka shauri langu mbele zake.
9 iYeye hutenda maajabu yasiyoweza kutambuliwa,
miujiza isiyoweza kuhesabika.
10 jYeye huipa nchi mvua,
huyapeleka maji kunyesha mashamba.
11 kHuwainua juu wanyonge,
nao wale waombolezao huinuliwa wakawa salama.
12 lHuipinga mipango ya wenye hila,
ili mikono yao isifikie ufanisi.
13 mYeye huwanasa wenye hekima katika hila yao,
nayo mipango ya wadanganyifu huifagilia mbali.
14 nGiza huwapata wakati wa mchana;
wakati wa adhuhuri hupapasa kama vile usiku.
15 oHumwokoa mhitaji kutokana na upanga ulioko kinywani mwao;
huwaokoa kutokana na makucha ya wenye nguvu.
16 pKwa hiyo maskini analo tarajio,
nao udhalimu hufumba kinywa chake.

17 q“Heri mtu yule ambaye Mungu humrudi;
kwa hiyo usidharau adhabu yake Mwenyezi.
Mwenyezi hapa ni jina la Kiebrania Shaddai (hapa na kila mahali katika kitabu hiki cha Ayubu).

18 sKwa kuwa hutia jeraha, lakini pia huyafunga;
huumiza, lakini mikono yake pia huponya.
19 tKutoka majanga sita atakuokoa;
naam, hata katika saba hakuna dhara litakalokupata wewe.
20 uWakati wa njaa atakukomboa wewe na kifo,
naye katika vita atakukomboa na pigo la upanga.
21 vUtalindwa kutokana na kichapo cha ulimi,
wala hutakuwa na sababu ya kuogopa maangamizi yatakapokujia.
22 wUtayacheka maangamizo na njaa,
wala hutakuwa na sababu ya kuwaogopa
wanyama wakali wa mwituni.
23 xKwa kuwa utakuwa na agano na mawe ya mashamba,
nao wanyama wa mwitu watakuwa na amani nawe.
24 yUtajua ya kwamba hema lako li salama;
utahesabu mali zako wala hutakuta chochote kilichopungua.
25 zUtajua ya kuwa watoto wako watakuwa wengi,
nao wazao wako wengi kama majani ya nchi.
26 aaUtaingia kaburini ukiwa na umri wa uzee mtimilifu,
kama masuke ya ngano yakusanywapo kwa wakati wake.

27 ab“Tumelichunguza hili, nalo ni kweli.
Hivyo lisikie na ulitendee kazi.”
Copyright information for SwhNEN