Psalms 75

Mungu Ni Mwamuzi

(Kwa Mwimbishaji: Kwa Ala Za Uimbaji Za Nyuzi. Zaburi Ya Asafu. Wimbo)

Ee Mungu, tunakushukuru,
tunakushukuru wewe,
kwa kuwa jina lako li karibu;
watu husimulia matendo yako ya ajabu.
Unasema, “Ninachagua wakati maalum;
ni mimi nihukumuye kwa haki.
Wakati dunia na watu wake wote inapotetemeka,
ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara.
Kwa wale wenye majivuno ninasema,
‘Msijisifu tena’,
kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu.
Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu;
msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’ ”
Hakuna ye yote atokaye mashariki wala magharibi
au kutoka jangwani
awezaye kumkweza mwanadamu.
Bali Mungu ndiye ahukumuye:
Humshusha huyu na kumkweza mwingine.
Mkononi mwa BWANA kuna kikombe
kilichojaa mvinyo unaotoka povu
uliochanganywa na vikolezo;
huumimina, nao waovu wote wa dunia
hunywa mpaka tone la mwisho.
Bali mimi, nitatangaza hili milele;
nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo.
10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote,
bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.
Copyright information for Neno