Isaiah 9

Kwa Ajili Yetu Mtoto Amezaliwa

1 aHata hivyo, hapatakuwepo huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Wakati uliopita aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataiheshimu Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, kando ya Yordani:

2 bWatu wanaotembea katika giza
wameona nuru kuu,
wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti,
nuru imewazukia.
3 cUmelikuza taifa,
na kuzidisha furaha yao,
wanafurahia mbele zako,
kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno,
kama watu wafurahivyo
wagawanyapo nyara.
4 dKama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani,
umevunja nira iliyowalemea,
ile gongo mabegani mwao na
fimbo yake yeye aliyewaonea.
5 eKila kiatu cha askari kilichotumiwa vitani,
na kila vazi lililovingirishwa katika damu
vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa,
vitakuwa kuni za kuwasha moto.
6 fKwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,
tumepewa mtoto mwanaume,
nao utawala utakuwa mabegani mwake.
Naye ataitwa
Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,
Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.
7 gKuongezeka kwa utawala wake na amani
hakutakuwa na mwisho.
Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi
na juu ya ufalme wake,
akiuthibitisha na kuutegemeza
kwa haki na kwa adili,
tangu wakati huo na hata milele.
Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote
utatimiza haya.

Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli

8Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo,
utamwangukia Israeli.
9 hWatu wote watajua hili:
Efraimu na wakazi wa Samaria,
wanaosema kwa kiburi
na majivuno ya mioyo,
10 i“Matofali yameanguka chini,
lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa,
mitini imeangushwa,
lakini tutapanda mierezi badala yake.”
11 jLakini Bwana amemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao
na kuchochea watesi wao.
12 kWaashuru kutoka upande wa mashariki
na Wafilisti kutoka upande wa magharibi
wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.

13 lLakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga,
wala hawajamtafuta Bwana Mwenye Nguvu Zote.
14 mKwa hiyo Bwana atakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia,
tawi la mtende na tete katika siku moja.
15 nWazee na watu mashuhuri ndio vichwa,
nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia.
16 oWale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha,
nao wale wanaoongozwa wamepotoka.
17 pKwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana,
wala hatawahurumia yatima na wajane,
kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu, nao ni waovu,
na kila kinywa kinanena upotovu.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.

18 qHakika uovu huwaka kama moto;
huteketeza michongoma na miiba,
huwasha moto vichaka vya msituni,
hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi.
19 rKwa hasira ya Bwana Mwenye Nguvu Zote
nchi itachomwa kwa moto,
nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto.
Hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake.
20 sUpande wa kuume watakuwa wakitafuna,
lakini bado wataona njaa;
upande wa kushoto watakuwa wakila,
lakini hawatashiba.
Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya mtoto wake mwenyewe:
21 tManase atamla Efraimu,
naye Efraimu atamla Manase;
nao pamoja watakuwa kinyume na Yuda.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,
mkono wake bado umeinuliwa juu.
Copyright information for SwhNEN