Psalms 106

Wema Wa Bwana Kwa Watu Wake

1 aMsifuni Bwana.

Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;
upendo wake wadumu milele.
2 bNi nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Bwana
au kutangaza kikamilifu sifa zake?
3 cHeri wale wanaodumisha haki,
ambao daima wanafanya yaliyo mema.
4 dEe Bwana, unikumbuke unapowatendea mema watu wako,
uwe msaada wangu unapowaokoa,
5 eili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako,
niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako,
na kuungana na urithi wako katika kukusifu.

6 fTumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda,
tumekosa na tumetenda uovu.
7 gWakati baba zetu walipokuwa Misri,
hawakuzingatia maajabu yako,
wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako,
bali waliasi kando ya bahari, Bahari ya Shamu.
8 hHata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake,
ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.
9 iAlikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka,
akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani.
10 jAliwaokoa mikononi mwa adui;
kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.
11 kMaji yaliwafunika adui zao,
hakunusurika hata mmoja.
12 lNdipo walipoamini ahadi zake,
nao wakaimba sifa zake.

13 mLakini mara walisahau aliyowatendea,
wala hawakungojea shauri lake.
14 nJangwani walitawaliwa na tamaa zao,
walimjaribu Mungu nyikani.
15 oKwa hiyo aliwapa kile walichoomba,
lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha.

16 pKambini walimwonea wivu Mose,
na pia Aroni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Bwana.
17 qArdhi ilifunguka ikawameza Dathani,
ikawazika Abiramu na kundi lake.
18 rMoto uliwaka katikati ya wafuasi wao,
mwali wa moto uliwateketeza waovu.

19 sHuko Horebu walitengeneza ndama,
na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma.
20 tWaliubadilisha Utukufu wao
kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani.
21 uWalimsahau Mungu aliyewaokoa,
aliyekuwa ametenda mambo makuu huko Misri,
22 vmiujiza katika nchi ya Hamu
na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu.
23 wKwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza:
kama Mose mteule wake,
asingesimama kati yao na Mungu
kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.

24 xKisha waliidharau ile nchi nzuri,
hawakuiamini ahadi yake.
25 yWalinungʼunika ndani ya mahema yao,
wala hawakumtii Bwana.
26 zKwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa
kwamba atawafanya waanguke jangwani,
27 aakuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa,
na kuwatawanya katika nchi zote.

28 abWalijifunga nira na Baali wa Peori,
wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai.
29 acWaliichochea hasira ya Bwana,
wakamkasirisha kwa matendo yao maovu,
nayo tauni ikazuka katikati yao.
30 adLakini Finehasi alisimama na kuingilia kati,
nayo tauni ikazuiliwa.
31 aeHili likahesabiwa kwake haki,
kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.

32 afKwenye maji ya Meriba, walimkasirisha Bwana,
janga likampata Mose kwa sababu yao;
33 agkwa maana walimwasi Roho wa Mungu,
na maneno yasiyofaa yakatoka midomoni kwa Mose.

34 ahHawakuyaangamiza yale mataifa
kama Bwana alivyowaagiza,
35 aibali walijichanganya na mataifa
na wakazikubali desturi zao.
36 ajWaliabudu sanamu zao,
zikawa mtego kwao.
37 akWakawatoa wana wao
na binti zao dhabihu kwa mashetani.
38 alWalimwaga damu isiyo na hatia,
damu za wana wao na binti zao,
ambao waliwatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani,
nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.
39 amWakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda;
kwa matendo yao wenyewe wakajifanyia ukahaba.

40 anKwa hiyo Bwana akawakasirikia watu wake
na akauchukia sana urithi wake.
41 aoAkawakabidhi kwa mataifa
na adui zao wakawatawala.
42 apAdui zao wakawaonea
na kuwatia chini ya mamlaka yao.
43 aqMara nyingi aliwaokoa
lakini walikuwa wamezama kwenye uasi,
nao wakajiharibu katika dhambi zao.

44 arLakini akaangalia mateso yao
wakati aliposikia kilio chao;
45 askwa ajili yao akakumbuka agano lake,
na kutokana na upendo wake mkuu akapooza hasira yake.
46 atAkawafanya wahurumiwe
na wote waliowashikilia mateka.

47 auEe Bwana Mungu wetu, tuokoe.
Tukusanye tena kutoka kwa mataifa,
ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,
na kushangilia katika sifa zako.

48 avAtukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Watu wote na waseme, “Amen!”

Msifuni Bwana.
Copyright information for SwhNEN