Psalms 56
Kumtumaini Mungu
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.
1 aEe Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
2 bWasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,
wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
3 cWakati ninapoogopa,
nitakutumaini wewe.
4 dKatika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.
Mwanadamu apatikanaye na kufa,
atanitenda nini?
5 eMchana kutwa wanayageuza maneno yangu,
siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.
6 fWananifanyia hila, wanajificha,
wanatazama hatua zangu,
wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.
7 gWasiepuke kwa vyovyote,
Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.
8 hAndika maombolezo yangu,
orodhesha machozi yangu katika gombo lako:
je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?
9 iNdipo adui zangu watarudi nyuma
ninapoita msaada.
Kwa hili nitajua kwamba Mungu
yuko upande wangu.
10Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Bwana, ambaye neno lake ninalisifu,
11katika Mungu ninatumaini, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
12 jEe Mungu, nina nadhiri kwako,
nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.
13 kKwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti
na miguu yangu kwenye kujikwaa,
ili niweze kuenenda mbele za Mungu
katika nuru ya uzima.
Copyright information for
SwhNEN