Song of Solomon 5

Mpenzi

1 aNimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu,
bibi arusi wangu;
nimekusanya manemane yangu pamoja
na kikolezo changu.
Nimekula sega langu la asali na asali yangu;
nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.
Marafiki

Kuleni, enyi marafiki, mnywe;
kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.

Shairi La Nne

Mpendwa

2 b cNililala lakini moyo wangu ulikuwa macho.
Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha:
“Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu,
hua wangu, asiye na hitilafu.
Kichwa changu kimeloa umande,
na nywele zangu manyunyu ya usiku.”
3Nimevua joho langu:
je, ni lazima nivae tena?
Nimenawa miguu yangu:
je, ni lazima niichafue tena?
4Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo;
moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.
5Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu,
mikono yangu ikidondosha manemane,
vidole vyangu vikitiririka manemane,
penye vipini vya komeo.
6 d eNilimfungulia mpenzi wangu,
lakini mpenzi wangu alishaondoka;
alikuwa amekwenda zake.
Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake.
Nilimtafuta lakini sikumpata.
Nilimwita lakini hakunijibu.
7 fWalinzi walinikuta
walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini.
Walinipiga, wakanijeruhi,
wakaninyangʼanya joho langu,
hao walinzi wa kuta!
8 gEnyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza:
kama mkimpata mpenzi wangu,
mtamwambia nini?
Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.
Marafiki

9Je, mpendwa wako ni bora kuliko wengine namna gani,
wewe uliye mzuri kupita wanawake wote?
Je, mpendwa wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani,
hata unatuagiza hivyo?
Mpendwa

10 hMpenzi wangu anangʼaa, tena ni mwekundu,
wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.
11Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote,
nywele zake ni za mawimbi
na ni nyeusi kama kunguru.
12 iMacho yake ni kama ya hua
kandokando ya vijito vya maji,
aliyeogeshwa kwenye maziwa,
yaliyopangwa kama vito vya thamani.
13Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo
yakitoa manukato.
Midomo yake ni kama yungiyungi
inayodondosha manemane.
14 jMikono yake ni fimbo za dhahabu
iliyopambwa kwa krisolitho.
Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyongʼarishwa
iliyopambwa na yakuti samawi.
15 kMiguu yake ni nguzo za marmar
zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi.
Sura yake ni kama Lebanoni,
bora kama miti yake ya mierezi.
16 lKinywa chake chenyewe ni utamu,
kwa ujumla yeye ni wa kupendeza.
Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu,
ee binti za Yerusalemu.
Copyright information for SwhNEN